Pages

Monday, April 18, 2011

SEKONDARI ZA KATA ZIMEFUTA JANGA LA UJINGA NCHINI

HABARI nyingi zimeibuka , kuhusiana na uwepo wa sekondari za kata nchini. Wachambuzi wa masuala ya elimu na baadhi ya Watanzania wanazizungumzia sekondari hizo, bila kuzingatia ukweli wa kile kinachotokea katika jamii zetu.

Baada ya matokeo ya mitihani ya kidato cha nne yaliyotolewa Januari mwaka huu na kuonesha wengi kufeli, wengi wameelekeza lawama kwa Serikali na kushutumu uwepo wa shule za kata.

Wanaolaumu wote wanachukua matokeo ya sekondari za kata za Dar es Salaam, ambako wazazi wengi ni wavivu wa kufikiri, wasiotoa maelekezo kwa watoto wao, wazazi wazembe na
waliojaa lawama kwa Serikali kwa kila kitu.

Ni kweli matokeo ya kidato cha nne si mazuri, lakini hebu tujiulize sababu tunazozitoa juu ya matokeo hayo. Je, wakati wanafunzi walipofaulu miaka ya nyuma, vitabu vilikuwepo vya kutosha?

Je, wakati wanafunzi wanafanya vema katika mitihani yao, Serikali iliingilia kati ili wafaulu? Pengine ni maswali mepesi lakini ni ya muhimu mkubwa kwa shule za kata. Wengi wanasema shule za kata ni janga kwa taifa, lakini wakati huo huo wanailazimisha Serikali iwabane wamiliki
wa shule binafsi, wapunguze karo za shule zao.

Tunaposema shule za kata ni janga, ina maana tupo tayari shule hizo zifutwe? Kama ndiyo lengo lenyewe, basi haya ni mawazo ya kihaini. Kwa sababu hakuna kizuri, ambacho hakikuanza na kasoro.

Kuzitukana shule za kata, kwamba ni janga la taifa ni mawazo ya wahaini, ambao kwao wanasubiri waletewe vinono mezani ili wajichane. Shule za kata katika Mkoa wa Ruvuma,
hususani katika wilaya za Mbinga na Songea, kwa kiasi fulani zimepunguza msongamano katika shule nyingine.

Katika hili, wabunge Jenista Mhagama wa Peramiho, Emmanuel Nchimbi wa Songea Mjini, Gaudence Kayombo wa Mbinga Mashariki na John Komba wa Mbinga Magharibi ni mashahidi wa hili nilisemalo.

Mkoa wa Ruvuma ulikuwa na shule chache. Kwa mfano, wanafunzi waliomaliza shule ya Msingi wilayani Mbinga walikuwa wakigombea nafasi za kujiunga na sekondari za Songea Boys, Songea Girls, Kigonsera na Mbinga Day.

Hata hivyo ni shule mbili tu Mbinga Day na Kigonsera, zilikuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi wengi. Sekondari nyingine zinazochukua wanafunzi ni Mahilo, Ruanda, Hagati na Lundo sekondari, lakini kutokana na msongamano mkubwa hazikutosha.

Hivyo, ilihitajika njia mbadala ya kupunguza msongamano huo, kwa kuanzisha sekondari za kata kadiri inavyowezekana. Kutokana na wingi wa wahitaji elimu ya sekondari, na idadi kubwa ya waliofaulu mitihani yao kwa wastani mzuri ambao walitakiwa kupangiwa shule ili
waendelee na elimu.

Je, hawa wangeachwa kwa sababu hakuna sekondari? Watoto wa masikini hawa wangeenda
wapi? Kwa sababu ukisema shule hizi ni janga la taifa na kusema zifutwe, maana yake unataka kuzalisha janga la wajinga.

No comments:

Post a Comment

About Rural 2 Urban Skoolz

My photo
Dar es Salaam, Tanzania