Ni mengi yamekuwa yakizungumzwa juu ya changamoto zinazozikumba shule za kata zilianzishwa chini ya serikali yetu ya awamu ya nne. Pamoja na utetezi unaofanywa na wanasiasa wa chama tawala juu ya kuhalalisha uwepo wa shule za kata, mpaka kufikia baadhi ya wabunge kuhalalisha wanafunzi wa shule hizo kupata daraja sifuri wakidai kuwa ni bora hao waliopata sifuri kuliko watoto ambao hawakuweza kupata fursa ya kusoma.
Binafsi naungana na watanzania wengi wanaosikitishwa na mwenendo mbovu wa shule zetu za kata ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa ukichangiwa na siasa chafu zinazoingilia hata taaluma za watu. siamini kuwa viongozi wetu na wataalamu wa sera; ambao ni washauri wa serikali; hawakuwa na muda wa kutosha kufanya tathmini ya kina kabla ya kutoa maagizo ya utekelezwaji wa mpango huu wa elimu.
Dhamira ya serikali inashindwa kufahamika juu ya mpango huu. Kama sehemu ya wananchi makini wanaoweza kuhoji mipango kama hii, nimekuwa nikijiuliza je, serikali ilitaka kuwa na shule nyingi sana, zenye changamoto nyingi na kupelekea watoto wa maskini kufeli sana kwa kuwa watoto wa waheshimiwa husoma shule bora zaidi?, je, serikali ilitaka kuwa na wanafunzi wengi zaidi wanaopata fursa ya kupata elimu bora ya sekondari karibu na maeneo wanayotoka?. Kuna maswali mengi kila mtu aweza kujiuliza.
Ikiwa nia ya serikali yetu ilikuwa kuboresha elimu kwa kuhakikisha wahitimu wengi zaidi wanaomaliza elimu ya msingi wanapata fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari basi hapakuwa na haja ya kuwa na shule za kata katika kila sehemu ya nchi yetu. Unapozungumzia kata ukiwa Dar es salaam ni tofauti sana na neno kata katika baadhi ya wilaya za vijijini, hiki ndio kitu ambacho serikali yawezekana haikukigundua katika mpango wake wa awali. Tofauti hii ndio inayopelekea upungufu wa walimu, maabara, maktaba, mazingira rafiki kwa walimu na wanafunzi, pamoja na changamoto zinginezo.
No comments:
Post a Comment