Na mwandishi wetu
SERIKALI ya Tanzania ina sifa ya kipekee, nayo ni kuwa bingwa wa kujisifu kwa mafanikio ya kitakwimu.
Zungumza na kiongozi yoyote kuhusu mafanikio katika sekta ya elimu hatosita kukutajia takwimu kubwa kubwa za idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa katika madaraja mbalimbali ya elimu.
Akishamaliza idadi ya wanafunzi, atakutajia utitiri wa shule ama vyumba vya madarasa hata kama baadhi ni mabanda tu yasiyo na sifa ya kutumiwa na wanafunzi.
Hutosikia habari za vitendea kazi vya kufundishia na kujifunzia kama vitabu, vifaa vya maabara na mengineyo yanayochagiza maendeleo ya elimu shuleni hususan upatikanaji wa elimu bora.
Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantum Mahiza alinukuliwa na gazeti hili akisema serikali imejipanga ipasavyo kuwapokea wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za serikali mwaka 2011.
Kilichonigusa hadi kufikia hatua ya kuandika makala haya ni kauli ya Mahiza ambayo kwa mtazamo wangu nafikiri, tayari serikali imeshajitabiria kuwa mwaka huu wahitimu wengi wa darasa la saba watafaulu.
Gazeti lilimnukuu akisema: “Wanafunzi wengi walifaulu mitihani yao ya majaribio, hicho ni kiashiria cha kufaulu vizuri katika mtihani huu wa taifa.Serikali imejiandaa kupokea wanafunzi wengi zaidi kuliko mwaka jana,” alisema.
Ni kwa sababu hii, alisema tayari serikali kuu imeshatoa agizo kwa halmashauri zote kuhakikisha vyumba vya madarasa vinaongezwa katika shule za sekondari za umma. Hata hivyo baadhi ya watu wanauliza wanafunzi hawa watafaulu au watafaulishwa?
Kama wanafunzi hawa wanafaulu kwa kuwa wana uwezo, kwa nini kumekuwepo na taarifa za mara kwa mara kuwa baadhi ya wanafunzi wa sekondari hawajui kusoma na kuandika? Ni wapi kunakofanyika uzembe huu?
Mimi nina wasiwasi wa kuwepo kwa ‘kamchezo’ fulani serikalini. Pia nina shaka aidha serikali hufanya makusudi kuchagua wanafunzi hata wasiostahili kwa kutunga mitihani chini ya kiwango ili watoto wengi zaidi wafaulu kwa lengo la kuiletea serikali sifa au mchakato wa kuchagua wanafunzi umegubikwa na kiasi kikubwa cha uzembe.
No comments:
Post a Comment